Alhamisi, 1 Mei 2014

WASICHANA 6000, MTWARA KUNUFAIKA NA MRADI WA HAKUNA WASICHOWEZA BAADA YA KUPATA ELIMU NA MISAADA YA VIFAA VYA KUJISITIRI WAKATI WA HEDHI.

Wasichana mkoani Mtwara wamenufaika na elimu ya afya pamoja na vifaa vitakavyowasaidia kujisitiri
wakati wa hedhi.

Elimu hiyo na msaada vimetolewa kupitia mradi wa ujulikanao Hakuna Wasichoweza unaotekelezwa na
asasi ya T-MARC Tanzania kwa ufadhili wa watu wa Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Kimarekani
USAID kwa ushirikiano na Vodacom Foundation.

 Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo kwa wasichana walengwa wa mradi, Meneja wa Mradi wa huo, Doris Chalambo alisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wasichana kama njia ya
uhakika ya kufanikisha maendeleo ya  jamii na Taifa.

 ‘’Awamu ya kwanza ya mradi huu imewafikiwa jumla ya wasichana 5000 katika shule za msingi za Mtwara na jumla ya wasichana 1000 walioko nje ya shule katika kata 17", alisema Doris.

Walengwa wa mradi huu ni wasichana wenye umri wa miaka 9 – 15. Jumla ya shule 24 zimefikiwa na mradi huu ambao pia umetoa mafunzo kwa walimu 40 wa shule na Wakunga wa jadi, makungwi/Nyakanga 34 wanaotoa elimu kwa wasichana wanaobalehe.

Pia alisisitiza kwamba elimu hii juu ya masuala ya hedhi itawezesha kuongeza uelewa wa jamii kwa ujumla juu ya umuhimu wa kuwasaidia wasichana ili waweze kuhudhuria masomo yao kwa ufanisi zaidi na kufikia malengo yao kimaisha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Vodacom Foundation, Yessaya Mwakifulefule alisema kuwa
elimu inayotolewa na mradi na mradi huo utaliwezesha Taifa kupunguza kasi ya maambukizi ya
mgonjwa ya kujamiiana ikiwemo maambukizi ya Virusi vya vinavyosababisha Ukimwi (VVU),
miongoni mwa vijana.

Mwakifulefule alisema kila msichana atakuwa akipatiwa pakiti mbili za vifaa hivyo kwa mwezi na zoezi hili litafanyika kwa muda wa miezi mitano mfululizo.

“Tunajivunia kuwa sehemu ya chachu ya maendeleo katika sekta ya elimu hususani mradi huu wa
Hakuna Wasichoweza ambao umelenga kunufaisha jumla ya wasichana 6000 waliopo na wasiopo
shuleni”, alisema Mwakifulefule.

Naye Mtaalamu wa Masuala ya Misaada kwa jamii kutoka Vodafone, Laura Turkington alisema mradi
unakuza ushiriki wa wadau mbali mbali katika kukuza viwango vya elimu pamoja na kutoa taarifa
sahihi kwa jamii kuhusu changamoto zinazowakabili wasichana katika kipindi cha balehe.

Aidha, T-MARC imetoatoa shukurani kwa Shirika la USAID ambalo limetoa msaada wa dola za
Kimarekani laki mbili (200,000)  kufadhili uanzishwaji wa mradi huu pamoja na Vodacom
Foundation ambayo imechangia shilingi milioni 160, kufanikisha awamu hii ya kwanza ya mradi.




 Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bw. Salumu Masalanga (katikati) akipokea msaada wa pedi kwa niaba ya  wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Maendeleo chini ya programu ya Hakuna Wasichoweza iliyofadhiliwa na Vodacom na T-MARC.

Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bw. Salum Masalanga (katikati) akikabidhi msaada wa pedi kwa Mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Maendeleo, Neema Mohamed chini ya programu ya Hakuna Wasichoweza iliyofadhiliwa na Vodacom na T-MARC.

Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Jamii Vodacom, Yesaya Mwakifulefule (kushoto) na Mratibu wa Mradi kutoka T-MARC Tanzania, Bi. Dorice Chalambo (wa pili kulia) kwa pamoja wakikabidhi msaada wa pedi kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Maendeleo chini ya programu ya Hakuna Wasichoweza iliyofadhiliwa na Vodacom na T-MARC.

Hakuna maoni: