Jumamosi, 2 Novemba 2013

WAWILI wafariki Dar.

WATU wawili wamekufa jijini Dar es Salaam katika matukio mawili tofauti likiwemo la Frank Benonyitu aliyekutwa amekufa chumbani kwake, huko maeneo ya Yombo Kiwalani, wilayani Temeke.

Kamanda wa Polisi Mkoa Ilala Marietha Minangi alisema tukio hilo lilitokea saa 9.45 alasiri, ambapo mwili wa marehemuhuyo ulikutwa ukiwa umelala ndani humo bila ya jeraha lolote.

Marietha alisema, kwa mujibu wa maelezo ya mke wa marehemu Consolata Kayenga alisema siku hiyo alimuacha mumewe akiwa peke yake hapo nyumbani kwao ambapo yeye alienda kwenye send off ya mama ya mdogo, huko maeneo ya Mbande Mbagara.

Alisema mke huyo aliporejea kutoka kwenye send off alikuta mlango wa chumba chao umefungwa kwa ndani, alipochungulia kwenye tundu la mlango alimuona mumewe amelala kitandani akiwa tayari ameshafariki.

Aidha, Marietha alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa ajili ya uchunguzi.

Katika tukio lingine, mkazi wa Chang'ombe Unubini Shaban Nyakimwili aligonwa na gari na kufariki papo hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke Anglibert Kiondo alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 6.30 mchana, huko katika makutano ya barabara ya Mandela na Mbozi.

Kiondo alisema gari lenye namba za usajili namba T460 AMA, aina ya fuso, lilimgonga Nyakimwili aliyekuwa anavuka barabara kutoka upande wa kulia kwenda kushoto na hatimaye kufariki papo hapo.

Kwa mujibu wa Kamanda Kiondo, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Temeke, huku upelelezi unaendelea ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Hakuna maoni: