Jumamosi, 23 Novemba 2013

NGUGI awataka wasomi waliopata elimu nje ya Afrika kuacha kuiga tamaduni za Ulaya.

MWANAHARAKATI na Mwandishi wa vitabu Ngugi wa Thiong'o akizungumza katika kongamano lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, jana.

BAADHI ya wasomi barani Afrika waliopata elimu katika nchi za magharibi wamekuwa wakitawaliwa na utamaduni wa nchi hizo, ikiwemo kuacha kutumia lugha zao.

Hayo yalisemwa jana, Dar es Salaam na mwanaharakati na mwanasihi kutoka Kenya , Profesa Ngugi wa Thiong’o kwenye kongamano lililofanyika ukumbi wa Nkuruma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema wasomi wamekuwa wakiacha kuendeleza lugha zao za Afrika, tofauti na wasomi wa zamani ambao walikuwa wanatumia lugha zao kuwa siraha katika mapambano ya kujikomboa katika mikono ya wakoloni.

“Utamkuta mwafrika ambaye amepata elimu katika bara la ulaya, hata jina anabadilisha na kuweka la kizungu au anatumia lugha ya kingereza wakati wote, hata hivyo si kwamba watu wasijifunze kingereza ila wanapotoka huko wabaki na utamaduni wao wa Afrika”. Alisema Profesa Ngugi.

Alisema ni vizuri kujua lugha nyingi zaidi lakini si kutekwa au kutawaliwa na lugha za mataifa ya ulaya kwani bado utakuwa mtumwa wa tamaduni.

Profesa Ngugi alisema wasomi Afrika wa enzi hizo walikuwa wakitumia lugha zao kuwa kiungo muhimu na kuzithamini ambapo walizitumia katika harakati za ukombozi katika bara la Afrika ingawa kuna baadhi walikuwa wanaona hazifai.

Alisema kuenea kwa Kiswahili duniani ni matokeo ya wasomi na viongozi ambao waliweka sera na nadharia kwa vitendo katika jamii.

“Hayati Mwalimu Julias Nyerere ameacha urithi kwa watanzania kwa kukiendeleza Kiswahili kuwa lugha inayofahamika kimataifa duniani sawa na lugha nyingine”. Alisema Ngugi.

Alisema Nyerere mmoja wa wasomi waliokifanya Kiswahili kuwa lugha ya taifa kwa vitendo ambapo alitumia hotuba mbalimbali kwa lugha hiyo.


Ngugi wa Thiong'o akiwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Rwekeza Mukandala katika ukumbi wa Nkulumah.

Hakuna maoni: