Jumamosi, 7 Desemba 2013

HAYA NI CHADEMA LINDI

Mwenyekiti aliyejiuzuru CHADEMA Mkoa wa Lindi Ally Chitanda amemjibu katibu Mkuu wa Chama hicho Dk. Wilbrod Slaa na kumwita ni mwenye tama na mbinafsi huku chama kikitafunwa na udini, ukabila na ukanda.

Chitanda alitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, Dar es Salaam, ambapo alisema kuhusu hoja hiyo ya udini, ukabila na ukanda ni kwamba kati ya wakurugenzi sita, watatu ni wenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro na wote sita hakuna hata Mwislamu.

Alisema watanzania kutambua kuwa Dk. Slaa ni mlevi wa madaraka  na ndio maana hata yeye aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa, Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa na Katibu wa Sekretarieti anamwita mtu mdogo katika chama.

“Ikiwa mimi ananiita mtu mdogo na nyazifa zangu hizo kwenye chama je, wanachama wa kawaida atawaitaje? Mimi nawathibitishia watanzania wenzangu mungu alitunusuru 2010, uchaguzi uliopita kwani Dk. Slaa ni mbinafsi na anatamaa.” Alisema Chitanda.

Akizungumzia kuhusu uhasama ulipo kati ya Zitto na Mwenyekiti Freeman Mbowe na Dk. Slaa, Chitanda alisema ulitokana na  Zitto kutaka kugombea uenyekiti wa chama hicho mwaka 2009.

Alisema uhasama huo uliongezeka baada ya Mbowe na Dk. Slaa kuwakumbatia watu ambao walikuwa wakimtukana Zitto, kwenye mitandao ya kijamii.

“Nasema Zitto hana kosa lolote linalofanana na adhabu aliyopewa na  chama hicho, hivyo Mbowe na Dk. Slaa wanajukumu la wajibu wa kusimamia haki na ukweli ndani ya CHADEMA.” Alisema Chitanda.

Aidha, Chitanda alizungumzia kuhusu hoja iliyotolewa na msemaji wa CHADEMA, Makene iliyomtaka aonyeshe barua ya uteuzi wa Katibu wa Sekretarieti alisema hoja hiyo inaonyesha ni namna Dk. Slaa alivyokuwa dhaifu katika utendaji wake wakazi.

Alisema nafasi hiyo alipewa mwaka 2010 na ilitokana na aliyetakiwa kufanya kazi hiyo ni Zitto, hivyo kutokana na kukabiliwa na majukumu mengi ya kikazi, akapendekezwa yeye atiuliwe kushika wadhifa huo ambapo sekretarieti ilithibitisha uteuzi huo chini ya uenyekiti wa Dk. Slaa.

“Uthibitisho wa kutosha ninao wa kuitumikia nafasi hiyo na ninayo baadhi ya maelekezo niliyokuwa nikipewa na Dk. Slaa na endapo sikua na wadhifa huo kwenye vikao vya sekretarieti, Kamati Kuu nilikuwa naingia kufanya nini?” alisema.

Jumamosi, 23 Novemba 2013

MBUNGE WA KIBAHA VIJIJINI ATOA VYETI KWA WAHITIMU WA MAFUNZO YA BODABODA

UKOSEFU wa elimu ya usalama barabarani kwa madereva wa pikipiki, ni chanzo kikuu cha ajali zinazotokea katika mkoa wa pwani, Kibaha.

Hayo yalisemwa jana, Mkoani humo na Mbunge wa Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa wakati akiwakabidhi vyeti madereva 65, walihitimu mafunzo ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki.

Jumaa alisema ajali nyingi za pikipiki zinazotokea ni kutokana baadhi ya madereva kutokujua na kuzingatia sheria za barabarani kwani wengi wao wanajifunzia mitaani.

"Bila elimu hiyo huwezi kuwa dereva mzuri na mwenyekutimiza kutimiza majukumu ya kazi ipasavyo na kuwataka waache ubishi na wazingatie sheria zote, ikiwemo kuvaa kofia ngumu, kutanua na kupakia abiria zaidi ya mmoja." alisema.

Aidha,Jumaa alisisitiza kwa wale ambao wamepata mafunzo hayo wakayatumie vizuri ili waonekane tofauti nawale ambao hawakufanikiwa kupata elimu hiyo.

Hata hivyo Mbunge huyo alisema yuko tayari kusaidia kuendelezwa kwa mafunzo hayo ili kuhakikisha ajali zinapungua katika mkoani hapo.

Kwa upande wa ASP Aisha Soud akisoma risala kwa niaba ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani wilayani Kibaha,Edward Mutailuka alisema mafunzo hayo yamekuwa na mafanikio kwakuwa ajali zimepungua.

Aisha alisema madereva ambao wanapata ajali kwa kipindi hiki wanakuwa hawajapata elimu na wengine hawana leseni za udereva.

WAZAWA JITOKEZENI KUWEKEZA KATIKA SEKTA YA GESI NA MAFUTA





KAIMU Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo na Petrol Tanzania (TPDC), Joyce Kisamo.


SHIRIKA LA Maendeleo la Petrol Tanzania (TPDC), imeziagiza kampuni za ndani zenye uwezo wa fedha na utaalam kuichangamkia fursa ya kupata zabuni kwa ajili ya kuwekeza katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia.


Kaimu Mkurugenzi wa shirika hilo Joyce Kisamo alisema hayo jana, Dar es Salaam, kuhusu mnada wa nne wa vitalu saba vya mafuta na gesi asilia vilivyoko baharini na kimoja kilichoko ziwa Tanganyika.

Alisema kampuni za ndani na nje zishiriki kupata zabuni ambazo zitafunguliwa mwakani, kwani TPDC na serikali imeweka utaratibu mzuri na kwa gharama nafuu ambazo kampuni hizo zinaweza kumudu gharama.

“Utaratibu uko wazi ambapo wazalendo na kampuni za nje zinaruhusiwa kushiriki katika mchakato huo ili mradi wawe na uwezo wa mtaji na kumudu gharama ambazo baadae zitarudishwa.” alisema Joyce.

Mkurugenzi huyo alisema vigezo vya kushiriki kwa kampuni za ndani zinazomilikiwa na wazawa vilivyowekwa na TPDC, kupata zabuni ni moja wapo kuwa na umiliki usipungue asilimia 50, ambazo zinajimudu kifedha na utaalam.

Pia, alisema hata kampuni za nje ambazo zinashirikiana na wazawa ambao watakuwa na umiliki wa zaidi ya asilimia 10, na watapewa kipaumbele kwani lengo ni kuhakikisha fedha zinabaki nyumbani badala kutoka nje.


Hata hivyo Joyce alisema kampuni za ndani si lazima zishiriki kataka uchimbaji bali yanaweza kuwekeza katika kutoa huduma mbalimbali kwa kampuni za uchimbaji ili mradi ziwe zimekidhi viwango vya kimataifa.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa utafutaji, Uzalishaji na Shughuli za Kiufundi Dk. Emma Msaky alisema mshiriki anaweza kulipia ada isiyorejeshwa, kugharamia vifurushi vya data katika vitalu vya baharini na ziwa Tanganyika.

Alisema waombaji hao watatakiwa kuonyesha taarifa za ununuzi ya vitalu hivyo yaani masharti ya zabuni husika katika kitalu alichonunua lakini anaweza kununua vitalu vyote, ambavyo vinagharimu bilioni za 6.

Aidha, Dk. Emma amewataka watanzania kuwekeza katika biashara hiyo ambayo ina faida kubwa duniani kote.


KAIMU Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo na Petrol Tanzania (TPDC), Joyce Kisamo akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani), Dar es Salaam kuhusu mnada wa nne wa vitalu saba vya mafuta na gesi asilia ambapo azitaka kampuni za ndani zijitokeze kuwekeza utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta. kulia ni Mkuu wa Manunuzi TPDC Edwin Riwa..


NGUGI awataka wasomi waliopata elimu nje ya Afrika kuacha kuiga tamaduni za Ulaya.

MWANAHARAKATI na Mwandishi wa vitabu Ngugi wa Thiong'o akizungumza katika kongamano lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, jana.

BAADHI ya wasomi barani Afrika waliopata elimu katika nchi za magharibi wamekuwa wakitawaliwa na utamaduni wa nchi hizo, ikiwemo kuacha kutumia lugha zao.

Hayo yalisemwa jana, Dar es Salaam na mwanaharakati na mwanasihi kutoka Kenya , Profesa Ngugi wa Thiong’o kwenye kongamano lililofanyika ukumbi wa Nkuruma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema wasomi wamekuwa wakiacha kuendeleza lugha zao za Afrika, tofauti na wasomi wa zamani ambao walikuwa wanatumia lugha zao kuwa siraha katika mapambano ya kujikomboa katika mikono ya wakoloni.

“Utamkuta mwafrika ambaye amepata elimu katika bara la ulaya, hata jina anabadilisha na kuweka la kizungu au anatumia lugha ya kingereza wakati wote, hata hivyo si kwamba watu wasijifunze kingereza ila wanapotoka huko wabaki na utamaduni wao wa Afrika”. Alisema Profesa Ngugi.

Alisema ni vizuri kujua lugha nyingi zaidi lakini si kutekwa au kutawaliwa na lugha za mataifa ya ulaya kwani bado utakuwa mtumwa wa tamaduni.

Profesa Ngugi alisema wasomi Afrika wa enzi hizo walikuwa wakitumia lugha zao kuwa kiungo muhimu na kuzithamini ambapo walizitumia katika harakati za ukombozi katika bara la Afrika ingawa kuna baadhi walikuwa wanaona hazifai.

Alisema kuenea kwa Kiswahili duniani ni matokeo ya wasomi na viongozi ambao waliweka sera na nadharia kwa vitendo katika jamii.

“Hayati Mwalimu Julias Nyerere ameacha urithi kwa watanzania kwa kukiendeleza Kiswahili kuwa lugha inayofahamika kimataifa duniani sawa na lugha nyingine”. Alisema Ngugi.

Alisema Nyerere mmoja wa wasomi waliokifanya Kiswahili kuwa lugha ya taifa kwa vitendo ambapo alitumia hotuba mbalimbali kwa lugha hiyo.


Ngugi wa Thiong'o akiwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Rwekeza Mukandala katika ukumbi wa Nkulumah.

Jumapili, 10 Novemba 2013

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Kinondoni akabidhi kadi kwa wanachama wapya zaidi 100.

MWENYEKITI wa UWT, Wilayani Kinondoni akimkabidhi kadi ya UWT, mmoja wa wanachama waliojiunga na umoja huo, leo wakati wa semina kwa viongozi wa tawi la Ubungo Msewe.


BAADHI ya wanachama wakiapa kuitumikia UWT, mara baadhi ya kukabidhiwa kadi kwa wanachama wapya zaidi ya 100.
 


Mwenekiti wa UWT, Kinondoni akiwaongoza wanachama kula kiapo cha kukitumikia chama na umoja huo, ambao unashika kasi katika jimbo la ubungo.


Florence akiwa mmoja ya mikutano katika mikutano ya UWT, Kinondoni kuwahamasisha wanawake na kuwaeleza namna ya serikali ya CCM, inavyoendelea kutimiza ilani ya yake.

Jumamosi, 9 Novemba 2013

WATENDAJI wasiowajibika katika kata na mitaa yao waondoke wenyewe.

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini amewaagiza maofisa utumishi na watendaji kata na mitaa kutekeleza majukumu ya kuziweka manispaa zao katika hali ya usafi na wakishindwa wataondolewa.

Sagini alitoa agizo hilo juzi, jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara ya kukagua hali ya usafi katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Alisema watendaji walioko katika kata na mitaa wasimamie kazi zao ipasavyo kwa kuzitumia sheria ndogo ndogo zilizopo ili kuhakikisha manispaa hiyo inakuwa katika hali ya uchafu.

Alisema maeneo ya mijini yanadhalisha taka nyingi kuliko vijijini, hivyo basi watendaji wasimamie majukumu yao ili kuondoa adha na endapo wakishindwa kusimamia watahamishiwa vijijini ambako hakuna uchafuzi wa mazingira.

“Wakakague kwenye maeneo ya wafanyabiashara ambao sehemu zao za biashara ni chafu wawaifungie au kuwapeleka mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake.” Alisema.

Alisema kata zinaweza kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi wakaokuwa na jukumu la kulinda na kuwakamata watu wenye tabia ya kuchafua mazingira kwa kumwaga maji au taka barabarani na kuwatoza faini.

Pia, Sagini amewaagiza wafanyabiashara ndogondogo na wenye maduka ambao wanapanga bidhaa zao pembeni mwa barabara kuacha tabia hiyo kwani wanawasumbua watembea kwa miguu.

Baadhi ya maeneo alitembelea katika manispaa hiyo ni Hospitali ya Mwananyamala, kituo kipya cha mabasi ya daradara kinachojengwa katika eneo la sim 2000 kilichoko kata ya Sinza, Shule ya Msingi Hekima, Tandale, soko la Tandale, machinjio ya kuku katika soko la Mtambani na Ofisi ya kata ya Magomeni.



KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Jumanne Sagini akizungumza na baadhi ya wagonjwa katika Hospitali ya Mwananyamala wakati wa ziara aliyoifanya katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.




TAMISEMI na Watendaji wa manispaa ya Kinondoni wakiangalia daraja la mlalakuwa ambalo limekuwa likilalamikiwa lilkitiririsha maji taka, hata hivyo viongozi hao walipotembelea walikuta liko katika hali nzuri ya usafi. 

WAFANYAKAZI katika soko la machinjio ya kuku la Mtambani wilayani Kinondoni wakiwa kazini.



Ray C akizungumza na Katibu Mkuu (TAMISEMI) Jumanne Sagini wakati alipofanya ziara katika Hospitali ya Mwananyamala.

Jumamosi, 2 Novemba 2013

MAMLAKA husika chukueni hatua kudhibiti hali usafi katika mazingira wanayoishi dinadamu.



CHEMBA ya maji taka inavyohatarisha afya za wapita njia katika eneo la buguruni sokoni, kwa wiki kadhaa chemba hiyo imekuwa ikitiririsha maji taka.

WATEMBEA kwa miguu wakipata taabu kwa kukanyaga maji taka ambayo yanatiririka kutoka kwenye moja chembe zilizoko katika eneo la Buguruni Sokoni.