Jumamosi, 7 Desemba 2013

HAYA NI CHADEMA LINDI

Mwenyekiti aliyejiuzuru CHADEMA Mkoa wa Lindi Ally Chitanda amemjibu katibu Mkuu wa Chama hicho Dk. Wilbrod Slaa na kumwita ni mwenye tama na mbinafsi huku chama kikitafunwa na udini, ukabila na ukanda.

Chitanda alitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, Dar es Salaam, ambapo alisema kuhusu hoja hiyo ya udini, ukabila na ukanda ni kwamba kati ya wakurugenzi sita, watatu ni wenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro na wote sita hakuna hata Mwislamu.

Alisema watanzania kutambua kuwa Dk. Slaa ni mlevi wa madaraka  na ndio maana hata yeye aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa, Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa na Katibu wa Sekretarieti anamwita mtu mdogo katika chama.

“Ikiwa mimi ananiita mtu mdogo na nyazifa zangu hizo kwenye chama je, wanachama wa kawaida atawaitaje? Mimi nawathibitishia watanzania wenzangu mungu alitunusuru 2010, uchaguzi uliopita kwani Dk. Slaa ni mbinafsi na anatamaa.” Alisema Chitanda.

Akizungumzia kuhusu uhasama ulipo kati ya Zitto na Mwenyekiti Freeman Mbowe na Dk. Slaa, Chitanda alisema ulitokana na  Zitto kutaka kugombea uenyekiti wa chama hicho mwaka 2009.

Alisema uhasama huo uliongezeka baada ya Mbowe na Dk. Slaa kuwakumbatia watu ambao walikuwa wakimtukana Zitto, kwenye mitandao ya kijamii.

“Nasema Zitto hana kosa lolote linalofanana na adhabu aliyopewa na  chama hicho, hivyo Mbowe na Dk. Slaa wanajukumu la wajibu wa kusimamia haki na ukweli ndani ya CHADEMA.” Alisema Chitanda.

Aidha, Chitanda alizungumzia kuhusu hoja iliyotolewa na msemaji wa CHADEMA, Makene iliyomtaka aonyeshe barua ya uteuzi wa Katibu wa Sekretarieti alisema hoja hiyo inaonyesha ni namna Dk. Slaa alivyokuwa dhaifu katika utendaji wake wakazi.

Alisema nafasi hiyo alipewa mwaka 2010 na ilitokana na aliyetakiwa kufanya kazi hiyo ni Zitto, hivyo kutokana na kukabiliwa na majukumu mengi ya kikazi, akapendekezwa yeye atiuliwe kushika wadhifa huo ambapo sekretarieti ilithibitisha uteuzi huo chini ya uenyekiti wa Dk. Slaa.

“Uthibitisho wa kutosha ninao wa kuitumikia nafasi hiyo na ninayo baadhi ya maelekezo niliyokuwa nikipewa na Dk. Slaa na endapo sikua na wadhifa huo kwenye vikao vya sekretarieti, Kamati Kuu nilikuwa naingia kufanya nini?” alisema.